Chuo cha Biashara (CBE) cha mkoa wa Dar es Salaam juzi kilitawazwa kuwa
mabingwa wapya wa fainali za taifa za mashindano ya mchezo wa pool kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu nchini baada ya kuibuka na ushindi wa magoli
13-5 dhidi ya chuo cha Mzumbe cha mkoa wa Mbeya katika mechi ya fainali.
Fainali za mashindano hayo yanayojulikana kama 'Safari Lager Higher
Learning Competition 2013' zilishirikisha vyuo vikuu vinane vilivyotwaa
ubingwa katika ngazi ya mikoa. Bendi ya African Stars (Twanga Pepeta)
ilitumbuiza fainali hizo zilizofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club,
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Chuo cha CBE kwa kutwaa ubingwa mashindano hayo yanayodhaminiwa na
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safari Lager,
walijinyakulia fedha taslim Sh. milioni 2.5 na kikombe cha ubingwa.
Mzumbe (Mbeya) kwa kushika nafasi ya pili waliondoka na Sh. milioni 1.5,
huku Mzumbe (Morogoro) walioshika nafasi ya tatu wakipata Sh. milioni
1.3. Chuo cha St. Augustine (Mwanza) kilizawadiwa Sh. milioni 1 kwa
kushika nafasi ya nne.
Vyuo vikuu vya Rucco (Iringa), Muccobs (Kilimanjaro), IAA (Arusha) na
St. John's (Dodoma) kila kimoja kilipewa kifuta jasho cha Sh.500,000 cha
kushiriki fainali hizo.
Ubingwa wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume) ulichukuliwa na Said Mohamed
wa chuo cha Rucco aliyezawadiwa Sh.300,000, George Tito wa chuo cha
Mzumbe (Morogoro) aliyeshika nafasi ya pili alipewa Sh.200,000 na Peter
Patrick wa IFM aliyeshika nafasi ya tatu alipata Sh.150,000. Walter
Thomson wa Mzumbe (Mbeya) alipewa Sh.100.000 kwa kushika nafasi ya nne.
Lilian Meory wa chuo cha CBE alitwaa ubingwa kwa mchezaji mmoja mmoja
(wanawake) na kuzawadiwa Sh.200.000, Agnes Jacob wa chuo cha St.
Augustine alishika nafasi ya pili na kuondoka na Sh.150,000, Amina Mhina
wa Mzumbe (Mbeya) alishika nafasi ya tatu na kupewa Sh.100,000 na Lemi
Jackson wa St.John's aliibuka katika nafasi ya nne na kupewa Sh.50.000.
Zawadi kwa washindi zilikabidhiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo
Tanzania (BMT), Dionis Malinzi aliyekuwa mgeni rasmi katika fainali
hizo.
0 comments:
Post a Comment