Home » » Niyonzima mali ya Yanga

Niyonzima mali ya Yanga


YANGA imemaliza uvumi uliotawala juu ya hatima ya kiungo wake nyota, Haruna Niyonzima kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili wa kuichezea timu hiyo.
Kwa kipindi cha zaidi ya mwezi, uvumi ulizagaa juu ya hatima ya kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda na vyombo vya habari kuandika kuwa anatakiwa na mahasimu wa timu hiyo, Simba na klabu ya Azam.
Lakini jana Yanga ilivunja ukimya kwa kumtambulisha kiungo huyo wa zamani wa APR kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kukipiga kwa mabingwa hao wapya wa soka wa Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Bin Kleb akimtambulisha kiungo huyo, aliwathibitishia waandishi wa habari kuwa wamempa mkataba wa miaka miwili utakaomfunga kwenye klabu hiyo mpaka mwisho wa msimu wa mwaka 2014/2015.
“Siwezi kusema amesaini mkataba wa thamani gani na lini na hiyo ni kutokana na utaratibu wetu wa kupenda kufanya mambo yetu kwa siri na umakini, lakini amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga,” alisema Bin Kleb katika mkutano kwenye Makao Makuu ya Yanga, Jangwani, Dar es Salaam.
Bin Kleb alisema alikuwa akishangazwa na taarifa za vyombo vya habari kwamba kiungo huyo amesaini kuichezea Simba na kusema hilo lisingewezekana kwani bado walikuwa wanahitaji huduma ya nyota huyo.
Niyonzima, ambaye pia kwa mashabiki wa Jangwani anafahamika kwa jina la Fabregas, akifananishwa na kiungo wa Barcelona na Hispania, Cesc Fabregas, alikiri kufuatwa na Simba ili kumsajili na kusema hiyo ni kawaida kwa mchezaji kama yeye, na kwamba amesaini Yanga kutokana na mapenzi yake kwa klabu hiyo.
“Ni hali ya kawaida kwa mchezaji kama mimi kufuatwa na timu na hata Simba walinifuata kunisajili, lakini nimeamua kusaini kuendelea kuichezea Yanga kwa mapenzi yangu,” alisema Niyonzima ambaye kwa mara ya kwanza alitua Jangwani msimu wa 2010/11, kwa mkataba wa miaka miwili.
Nahodha huyo wa kikosi cha timu ya Taifa, Amavubi, alisema baada ya kuisaidia Yanga kunyakua ubingwa msimu huu, alihitaji muda kidogo wa kupumzika kabla ya kufanya uamuzi wa hatima yake na kuongeza kuwa lengo ni kuisaidia timu kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Katika msimu uliomalizika, Niyonzima alikuwa nyota wa kikosi cha Ernie Brandts na kuisaidia kutwaa ubingwa uliokuwa ukishikiliwa na watani wao, Simba, hata kabla ya ligi kumalizika.
Wakati Niyonzima akiamua kubaki Yanga, tayari mabingwa hao wamemrejesha kundini mshambuliaji wake wa zamani, Mrisho Ngassa ambaye msimu uliomalizika alikuwa akiichezea Simba kwa mkopo akitokea Azam FC aliyojiunga nayo baada ya kuondoka Jangwani.

0 comments:

Post a Comment

Blog Archive

Popular Posts

.

CHAT BOX

My Blog List

 
Support : BONGOCLANTZ
Copyright © 2013. KANGAROO - All Rights Reserved
Template Created by EDDIE SUCRE
Proudly powered by Blogger