Latest Article Get our latest posts by subscribing this site

Stars, Morocco kuumana saa 5 usiku

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah
Mechi ya marudiano ya ya Kundi C la kuwania kufuzu kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia kati ya timu ya taifa ya Morocco (Simba wa Atlas) na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itachezwa Jumamosi usiku jijini Marrakech, Morocco, imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema kuwa mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 3:00 usiku kwa saa za jiji la Marrakech muda ambao itakuwa saa tano usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Osiah huyo alisema kuwa kikosi cha wachezaji 21 cha Taifa Stars jana kiliwasili salama jijini Marrakech kikitokea Ethiopia ambako kilicheza mechi ya kimataifa ya kirafiki inayotambuliowa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) dhidi ya timu ya timu ya taifa ya Sudan kwenye Uwanja wa Addis Ababa Jumapili. Timu hizo zilitoka suluhu.

Alisema kuwa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia hoteli ya Pullman ambayo pia ilikaa timu ya taifa ya Ivory Coast ilipokwenda kucheza dhidi ya Morocco na kwamba washambuliaji wawili wa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu walitarajiwa kuwasili jana saa 8 mchana wakitokea Maputo, Msumbiji ambapo timu yao ya TP Mazembe ilikuwa na mechi ya Kombe la Shirikisho.

"Timu itarejea nchini Juni 9 (Jumapili) kujiandaa kwa mechi nyingine ya marudiano ya Kundi C dhidi Ivory Coast itakayochezwa nchini (Tanzania) wiki moja baadaye (Juni 16)," alisema Osiah.

Katika mechi ya awali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu, Stars iliibuka na ushindi wa 3-1. Shukrani kwa magoli ya Samatta, aliyefunga magoli mawili na Ulimwengu.

Mabingwa wa Afrika wa mwaka 1992, Ivory Coast, wanaongoza msimamo wa kundi hilo wakiwa na pointi 7, moja nyuma ya Tanzania wanaokamata nafasi ya pili wakifuatwa na mabingwa wa Afrika mwaka 1976, Morocco, wenye pointi mbili huku Gambia wakishika mkia baada ya kuambulia pointi moja tu baada ya kila timu kucheza mechi tatu.
 

Kinana: Bora kuwa na wana-CCM wachache wazuri kuliko wengi walio hovyo

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema ni bora chama hicho kuwa na wanachama wachache walio wazuri kuliko kuwa nao wengi walio hovyo.

Kiongozi huyo wa CCM, alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa viongozi wa matawi na mashina wa chama hicho, uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea juzi.

Akitoa hotuba yake mbele ya mamia waliohudhuria mkutano huo, Kinana alisema si kwamba CCM ilikuwa imeshindwa katika kata sita mjini Songea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, bali ni wana-CCM wenyewe ndio waliopoteza.

“Sio kwamba CCM ilikuwa imeshindwa kushika kata hizo bali ni baadhi ya wana-CCM ambao ni wabinafsi wenye kufikiri kuwa wengine hawawezi kuongoza isipokuwa wao ndio waliokabidhi kata hizo kwa wapinzani” alisema na kuongeza:

 “Safari hii katika Uchaguzi Mkuu ujao tutakuwa wakali, bora tuwe na wana-CCM wachache walio wazuri kuliko kuwa na wengi lakini wa hovyo. Tutajiandaa kwa chaguzi zijazo kwa kupeana madarasa.”

Alisema ni marufuku kwa watendaji wa chama hicho kuwa mawakala kwa watu wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Kinana aliahidi kufanya ziara rasmi katika mkoa wa Ruvuma mwezi ujao baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan, aliuambia umati uliohudhuria kwamba, ili kusimamjia utekelezaji wa ahadi ambazo chama hicho kiliwahaidi Watanzania ili  mwaka 2015 kiwe na la kuwaambia wananchi.

Kinana akiwa mkoani humo kwa ziara ya siku moja alishiriki shughuli maalumu ya kuwakabidhi nishani ya mwenge wa uhuru wapiganaji uhuru wa Tanganyika kwa niaba ya Rais kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam.

Kibanda ana siri moyoni

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), Absalom Kibanda, akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, amerejea nchini kutoka Afrika Kusini alikokwenda kutibiwa, huku akiwa na siri moyoni kuhusu kilicho nyuma ya matukio mabaya yaliyowasibu baadhi ya waandishi wa habari, akiwamo yeye, ambayo ameahidi kuisema iwapo Mungu atampa uzima.

Alisema atafanya hivyo ili kuliokoa taifa, wanahabari wenzake na Watanzania kwa jumla, ili kuwasaidia wasiingie kwenye madhila, maumivu na mateso kama yale yaliyompata.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006 Limited, aliwasili nchini jana saa 7.55 mchana, akitokea Hospitali ya Milpark nchini humo, ambako alilazwa kwa miezi mitatu kisha kukaa hotelini kwa muda, baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam, Machi 5, mwaka huu.

Katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kumkata kidole, kumjeruhi kwa kitu kizito kichwani na kumharibu jicho la kushoto.

Baada ya tukio hilo, Machi 6, mwaka huu, Kibanda alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na baadaye katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), jijini Dar es Salaam.

Kisha  alipelekwa Afrika Kusini na kulazwa katika Hospitali ya Milpark, jijini Johannesburg.

Kibanda alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam jana na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa mamia ya wakazi wa Dar es Salaam, wakiwamo wahariri, waandishi na wananchi wengine.

Alisema akiwa Afrika Kusini, alipata taarifa nyingi kuhusiana na tukio lake na mengine yaliyowasibu wanahabari wengine nchini.

Kibanda alisema hataki kufanya makosa ya watu wengine na kwamba, yeye mwenyewe anakusudia kuyasemea hayo kila wakati.

“Katika matukio yangu na mengine, kama Mungu atanipa uzima nitalisemea. Tumekuwa tukipata taarifa nyingi,” alisema Kibanda.

Alisema alipouawa mwandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daud Mwangosi, alishiriki katika kutoa tamko la TEF lililokuwa la pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Pia alishiriki katika kufuatilia matukio mbalimbali ya waandishi kuumizwa au kujeruhiwa, likiwamo lile lililomsibu Shaban Matutu (Tanzania Daima) na Mnaku Mbani (Business Times).
“Nataka kuwahakikishia wanahabari wenzangu, kwamba, matukio yote haya si ya bahati mbaya,” alisema Kibanda.

Alisema wakati akiyapitia na kuyaangalia matukio ya wanahabari wenzake, hakujua hata siku moja kwamba, pengine na yeye kama angefikwa na matukio hayo.

“Nawaomba wanahabari wenzangu tufanye lolote tunaloweza kuhakikisha tukio la Kibanda linakuwa la mwisho. Matukio ya watu kupanga njama au kula njama na kujeruhi watu,” alisema Kibanda.

Kibanda alisema tukio la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, linafanana sana kimazingira na kimkakati na tukio lake.

Kibanda alisema akiwa hospitali Afrika Kusini, serikali ilituma mpelelezi, ambaye ni afisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi kuzungumza naye juu ya janga lililomkuta.

Pia alisema hataki kabisa kuwa mbinafsi kwa sababu anajua kwamba, mpaka sasa wanahabari na Watanzania kwa jumla wanashuhudia ukimya miongoni mwa vyombo mbalimbali vya dola unaoendelea kuhusu hatima ya uchunguzi wa tukio lake.

Kibanda alisema kinyume cha ukimya huo, vyombo hivyo viliahidi kwamba, vitalifanyia kazi tukio lake kwa kina na hatimaye watu waliohusika kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Alisema kabla hajaondoka hospitali, alitembelewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna (ACP) Suleiman Kova.

Kwa mujibu wa Kibanda, ahadi ya kulifanyia kazi tukio lake alipewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alipomtembelea hospitali Afrika Kusini, kwamba serikali itafanya lolote inaloweza.

“Bado namuuliza Mungu kwanini aliruhusu niwe hai hadi leo? Kama kuna ujumbe wa uhai wangu leo nina wajibu ninaotaka kuutimiza ili kuliokoa taifa langu, wanahabari wenzangu na Watanzania wengine wasiingie katika madhila, maumivu na mateso makali, ambayo nimepata,” alisema Kibanda.

Alisema ana kila sababu ya kufanya jambo, ambalo litawatoa Watanzania hapa walipo sasa.
“Kwa sababu hiyo nasema ndugu zangu, msimlilie Absalom Kibanda. Ililieni nchi yetu, ambayo katika kipindi cha miaka karibu nane ya utawala wa awamu nne, matukio ya namna hii yanaendelea kushamiri na hakuna linalofanyika,” alisema Kibanda.

Alisema akiwa Afrika Kusini, alisoma taarifa na kusikia kauli mbalimbali kutoka kwa wanasiasa, wanahabari na watu wengine kuhusu tukio lake.

Kibanda alisema la mwisho alilolisoma lilikuwa ni tamko la TEF, ambalo alisema walifanya kazi kubwa, ikiwa ni pamoja na kuandika muhtasari mzito sana.

Alisema zaidi ya hivyo, TEF walisafiri kwenda Afrika Kusini kuzungumza naye ingawa wakati huo alikuwa na maumivu makali kulinganisha na hivi sasa, lakini walifanikisha kazi yao na matokeo ameyaona.

Kibanda alisema: "Kama utasoma ripoti ya TEF, utagundua kwamba, kuna mambo mengi yaliyo nyuma ya ripoti hiyo."

Kabla ya kuanza kuzungumza hayo, Kibanda alibubujikwa machozi baada ya kushuhudia umati mkubwa wa watu waliofika uwanjani hapo kumpokea.

Baadhi wanahabari walibeba mabango yenye ujumbe wa kumkaribisha nyumbani na kuvihoji vyombo vya dola kuhusu hatima ya uchunguzi wa tukio lake.

Kibanda alisema ametoa machozi kwa sababu ya mshikamano mkubwa aliouona jana katika mapokezi yake.

Aliwashukuru wahariri, wanahabari, vyombo vyote vya habari na Watanzania kwa jumla kwa moyo wa ushirikiano na mshikamano waliouonyesha kufuatia matukio yaliyomsibu.

Pia alimshukuru Mwenyekiti wa Chama Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, kwa msaada mkubwa alioutoa kwake.

Alisema bado ana maumivu ya mwili, lakini hana maumivu ya roho na kuwaambia wanahabari na Watanzania kwamba, wana wajibu wa kuliokoa taifa kwani limepita katika kipindi kigumu.
 

Mbunge wa CCM ailipua serikali matokeo mabaya kidato cha nne

Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina
Kasi ya wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kukosoa utekelezaji wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete inazidi kuongezeka ndani ya Bunge.

Jana, Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina, aliikosoa serikali hiyo kwa kuyafuta matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2012, kisha kuyatangaza utangaza upya hivi karibuni.

Ntukamazina ambaye kitaaluma ni Mwalimu, alisema hatua hiyo ni ya kisiasa zaidi na mfano wa ‘danganya toto’ inayofanywa na serikali kwa umma.

Ntukamazina alisema hayo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2013/2014, iliyowasilishwa na waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa.

Alisema matokeo yanapofutwa, kinachofuata ni kufanyika upya na si kuyapitia (matokeo hayo)  kisiasa na kuyatangaza kwa wananchi.

Mbunge huyo alisema haifai kwa serikali kufanya siasa kwa mambo ya msingi kama elimu, na kukumbusha kuwa hata mtawala wa mwisho wa kikoloni kuondoka nchini alitahadhalisha hivyo.

Alisema, mtawala huyo, Gavana  Richard Turnbull, (wakati akiondoka) alimwambia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa anaweza kufanya siasa kwa mambo yote ya kijamii isipokuwa elimu.

Ntukamazina alielezea kushangazwa na hatua iliyofikiwa na Dk Kawambwa, kutangaza matokeo hayo kinyume cha taratibu. Alisema mamlaka yenye kutangaza matokeo hayo yapo kwa Baraza la Mitihani

Hata hivyo, Ntukamazina alisema jamii ina wajibu wa kushiriki kurekebisha mfumo wa elimu na kuinua kiwango cha ufaulu, kupitia malezi bora na kuwaepusha watoto dhidi ya tamaduni za kimagharibi.

“Nimekuwa Mwalimu tangu mwaka 1973, sijawahi kumuona Waziri akitangaza mitihani, hiyo ni kazi ya Baraza la Mitihani… msiingie jikoni, mtaungua,” alionya.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Naomi Kaihura, alisema kinachokwamisha ufanisi katika mambo ya msingi ya jamii kama elimu, ni kwa baadhi ya wabunge kuwa ‘vigeugeu’.

Alisema wabunge wanapokuwa kwenye Kamati za Bunge ama nje ya ukumbi huo, wanaongea mambo ya msingi yenye maslahi, lakini wanapoingia bungeni wanachangia tofauti, huku wakiwalinda waovu na uovu.

Nimefundisha 40 yrs.  Miporomoko na mianguko ya elimu nimeiona na kuishuhudia. Nchi ni wamoja, tukimbie mapepo, mahali hapo tutaongea lugha inayoeleweka.

Mbunge wa Mchinga (CCM), Said Mtanda, alishutumu mgawanyo usio sawa wa ukarabati wa shule na kusema imeupendelea zaidi mkoa wa Kilimanjaro.
CHANZO: NIPASHE

Vigogo wanaojihusisha na ujangili kutajwa hadharani

Naibu Waziri Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
Serikali imesema haitasita kuwataja hadharani vigogo ama wageni watakaokamatwa wanaofadhili na kusafirisha pembe za ndovu kwa njia ya kificho kwenda Bara la Asia na nchi za Kiarabu baada ya tembo kuuawa kwa njia haramu na kisha mazao yake kusafirishwa nje ya nchi.

Naibu Waziri Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema hayo wakati wa kikao cha wadau wa ulinzi wa maliasili na utalii, ambacho pamoja na mambo mengine kimekutana kujadili wimbi la ujangili wa tembo katika hifadhi zilizopo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Alisema mpango huo wa kuwaumbua baadhi ya watu wanaofadhili ujangili ama kusafirisha meno ya tembo kwenda nchi za Kiarabu na China, utakolezwa na mbinu mpya za kiintelijensia ambazo zitatumika katika ‘Operesheni Uhai’ ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

“Wanaofadhili shughuli za ujangili tutawatangaza majina yao hadharani katika kukabiliana na tatizo hili. Lakini pia wageni wote watakaokamatwa nchini kutokana na ujangili tutawafukuza ndani ya saa 24 tena watapaswa kulipa nauli za ndege kwa gharama zao baada ya kutumikia adhabu watakazopata kwa mujibu wa sheria,” alisema Nyalandu.

Alisema hivi sasa wimbi la ujangili nchini limekuwa kubwa kutokana na majangili hao kudaiwa kusaidiwa na baadhi ya wafanyakazi walioko kwenye vitengo vya ulinzi na usalama kwa kuwa suala zima la usafirishaji wa pembe za ndovu hauwezi kuvuka kwenye mikoa husika pamoja na hifadhi zetu hadi kwenda bandarini wasikamatwe au kufahamika kama baadhi ya watendaji hawausiki.

Alisema ujangili wa tembo unaongezeka kila mwaka na kwamba hali hiyo  inahusisha mtandao mkubwa wakiwepo wafanyakazi wanaozunguka maeneo hayo, ambapo inasemekana kuwa kila mwaka tembo 10,000 wanauawa, kitu ambacho kinahatarisha usalama wa tembo hao kuendelea kuwepo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Dk. Allani Kijazi, alisema katika kukabiliana na ujangili kwenye mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Dodoma, wadau wataunda kikosi kazi ambacho kitapambana na ujangili hasa katika hifadhi ikiwemo Ruaha ambayo kwa sasa ndiyo hifadhi kubwa nchini.
CHANZO: NIPASHE

Twanga kusherehekea miaka 15

mkurugenzi wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Asha Baraka
Bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta' inatarajia kufanya onyesho la sherehe za kutimiza miaka 15 ya bendi hiyo pamoja na uzinduzi wa albamu mpya ya bendi hiyo iitwayo 'Nyumbani ni Nyumbani' Juni 30 mwaka huu kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini, mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka, alisema kuwa maandalizi ya sherehe hizo yanaendelea vyema na kwamba kabla ya kuzindua albamu hiyo ya 12 usiku, asubuhi kutakuwa na shughuli mbalimbali za michezo zitakazowahusisha wadau na wapenzi wa bendi hiyo.

Asha alisema kuwa ndani ya miaka 15 ya kuwapo kwa bendi hiyo wamekumbana na changamoto mbalimbali ambazo zimemsaidia kuiimarisha na kubaki kwenye soko la muziki.

Alisema pia siku ya uzinduzi huo wanatarajia kuuza CD za albamu yao ya 11 iliyozinduliwa mwaka jana lakini mauzo yake yalisimama kufuatia kukamatwa kwa CD bandia siku moja baada ya uzinduzi.

"Tunatarajia kuwa na ujio tofauti katika uzinduzi na sherehe za miaka 15, pia napenda kuwaambia wapenzi wa muziki wa dansi kuwa muziki huu haujashuka ila haujapata nafasi ya kutangazwa, tunawaomba wamiliki wa vituo vya redio na televisheni watusaidie kwani bila kuonekana au kusikika muziki hauwezi kukua," alisema Asha.

Alisema uzinduzi wa albamu ya 'Fainali Uzeeni' iliyobebwa na wimbo huo uliotungwa na Jesca Charles, kuwa ndiyo uliovunja rekodi kwa onyesho lake kuhudhuriwa na mashabiki wengi na vile vile albamu hiyo kuuza nakala nyingi.

Alieleza kwamba suala la wanamuziki kuhama na kurejea katika bendi hiyo kwake halimsumbui na anajivunia kwa sababu wanamuziki wake wanafuatwa kutokana na wao kupika wanamuziki bora na kazi hiyo ndiyo wanaendelea kuifanya.

Wakati huo huo, Asha jana alitangaza kuzindua rasmi kwa studio mpya ya kurekodi nyimbo za muziki na filamu iitwayo Flavour Inc iliyopo jijini Dar es Salaam.

Alisema studio hiyo iliyoko chini ya mtayarishaji, Yunick Bulla 'Awax', itakuwa inarekodi nyimbo za aina mbalimbali na lengo lake ni kuwapa nafasi wasanii chipukizi kutengeneza kazi zao kwa gharama nafuu na vile vile kuwasaidia kuzitangaza kazi hiyo.

Joh Makini apagawisha tamasha la Coke Zero

Nyota wa muziki wa hip hop, Joh Makini 
Wakazi wa Jiji la Arusha na vitongoji vyake walijitokeza kwa wingi katika viwanja wa Soweto Jumamosi iliyopita kushuhudia wasanii wa muziki wa kizazi kipya akiwamo mkali wa hiphop nchini, Joh Makini wakifanya vitu vyao katika tamasha la Coke Zero. 

Tamasha hilo lilikuwa maalum kwa ajili wa uzinduzi wa kinywaji kipya cha Coca-cola Zero kinachotolewa na kampuni ya kutengeneza na kusambaza vinywaji baridi jamii ya Coca-Cola ya Bonite Bottlers yenye makao yake mjini Moshi.

Burudani hiyo ya aina yake ilianza saa nane mchana kwa vijana waendesha pikipiki kuonyesha umahiri wao wa kutawala chombo hicho cha moto kabla ya wasanii wanaoinukia wa hip hop, Paul Mushi na Juma Abdallah, kupanda stejini na kupokewa kwa shangwe na maelfu ya wapenzi wa muziki waliojitokeza kushuhudia tamasha hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika tukio hilo, Mkurungenzi Mkuu wa Mauzo wa kampuni ya Bonite Bottlers, Christopher Loiruk, alisema kampuni yake imeandaa tamasha hilo kwa ajili ya kuitambulisha Coke Zero na pia kuburudika pamoja na wateja wake.

"Bonite Bottlers tumekuwa mstari wa mbele katika kudhamini michezo na kuendeleza vipaji vya vijana, na leo tumeona kikundi kipya kabisa cha muziki wa hiphop kikipata nafasi ya kuonyesha umahiri. Wapenzi wa muziki watakubaliana nami kwamba kama vijana hawa wataendelea kupewa fursa na kuwezeshwa watakuwa wasanii wakubwa sana nchini," alisema Loiruk.

Naye Meneja Bidhaa ya Coca-Cola Tanzania, Maurice Njolowa alisema nia ya kampuni yake ni kuweka kinywaji kipya cha kampuni hiyo cha Coke Zero karibu na vijana na kwamba kuandaa tamasha la bure kama hilo ndiyo njia nzuri ya kuwa karibu nao.

Tamasha hilo ni muendelezo wa matamasha ya Coke Zero yaliyoanzia Coco Beach jijini Dar es Salaam wakati kinywaji hicho kisicho na sukari kilipozinduliwa Machi mwaka huu. Tamasha jingine la Coke Zero litafanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
 

Mwili wa Ngwair kutua leo saa 8

Albert Mwangweha a.k.a Ngwair
Mwili wa msanii Albert Mwangweha a.k.a Ngwair unatarajia kuingia nchini leo majira ya saa 8 mchana kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini (South Africa Airways).

Akizungumza na NIPASHE jana msemaji wa Kamati ya Mazishi, Adam Juma alisema kibali cha kifo cha msanii huyo tayari kimekamilika na akawashukuru wote waliowezesha mwili huo kuwasili.

"Kila kitu kipo sawa na tunamshukuru Mungu kwa kweli kwamba sasa ndugu yetu atawasili nchini tayari kwa kuzikwa, ni jambo la heri kwa kweli," alisema Adam.

Adam alisema kuwa kamati yake inawaomba wapenda muziki wote nchini kwenda kupokea mwili wa msanii huyo mkali ya 'freestyle' pindi utakapowasili.

"Baada ya mwili huo kuwasili nchini, moja kwa moja utakwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kesho Jumatano utaagwa katika viwanja vya Leaders Club na hatimaye safari ya kuupeleka mwili huo katika nyumba yake ya milele mkoani Morogoro itaanza," alisisitiza Adam.

Taarifa za kuletwa mwili huo nchini zilileta faraja kwa familia ya marehemu ambapo juzi msiba wa familia ulipo Mbezi eneo la Goigi, wanafamilia walionekana kusikitishwa na kuchelewa kufika mwili huo.

Juzi msemaji wa kamati hiyo, Adam Juma alitoa kauli ya kukata tamaa baada ya kuulizwa na gazeti hili kuwa ni lini mwili wa msanii huyo utawasili.

"Kwa kweli sina la kusema, mimi naona tuendelee kuvuta subira, mi' mwenyewe sielewi nashindwa hata kula....," alisema Adam.

Akizungumza na NIPASHE jana msanii wa siku nyingi wa muziki wa hiphop nchini na rafiki mkubwa wa marehemu, Jaymoe alisema kuwa angalau moyo umetulia baada ya kusikia kuwa mwili wa rafiki yake kipenzi utawasili nchini. "Ni furaha kwangu hata kwa familia yake haswa bi mkubwa wake (mama yake) kwani kule ni mbali nadhani baadhi ya watu ilifika kipindi walikata tamaa baada ya kuona siku zinakwenda na kule ni mbali....kamati ipo makini na mwili utakuja...".

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, ambaye amekuja nchini kwa ajili ya msiba huo na kwenda kuwatembelea wana familia jijini Dar es Salaam, alisema juzi kwamba kuchelewa kwa mwili huo kulisababishwa na taratibu tofauti za nchi hiyo katika kutoa kibali cha vifo.

Ngwair aliyekwenda nchini Afrika Kusini kufanya maonyesho, alifariki dunia usingizini nyumbani alipofikia huku msanii aliyeambatana naye akilazwa hospitalini huku sababu kilichowakuta kikiwa bado ni giza nene.

Balozi Msuya alisema vipimo vimeshatoka na vimekabidhiwa kwa familia ambayo itaamua kama ivitoe kwa umma ama isivitoe.  
 

CBE mabingwa pool vyuo vikuu taifa

Chuo cha Biashara (CBE) cha mkoa wa Dar es Salaam juzi kilitawazwa kuwa mabingwa wapya wa fainali za taifa za mashindano ya mchezo wa pool kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 13-5 dhidi ya chuo cha Mzumbe cha mkoa wa Mbeya katika mechi ya fainali.

Fainali za mashindano hayo yanayojulikana kama 'Safari Lager Higher Learning Competition 2013' zilishirikisha vyuo vikuu vinane vilivyotwaa ubingwa katika ngazi ya mikoa. Bendi ya African Stars (Twanga Pepeta) ilitumbuiza fainali hizo zilizofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Chuo cha CBE kwa kutwaa ubingwa mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safari Lager, walijinyakulia fedha taslim Sh. milioni 2.5 na kikombe cha ubingwa.

Mzumbe (Mbeya) kwa kushika nafasi ya pili waliondoka na Sh. milioni 1.5, huku Mzumbe (Morogoro) walioshika nafasi ya tatu wakipata Sh. milioni 1.3. Chuo cha St. Augustine (Mwanza) kilizawadiwa Sh. milioni 1 kwa kushika nafasi ya nne.

Vyuo vikuu vya Rucco (Iringa), Muccobs (Kilimanjaro), IAA (Arusha) na St. John's (Dodoma) kila kimoja kilipewa kifuta jasho cha Sh.500,000 cha kushiriki fainali hizo.

Ubingwa wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume) ulichukuliwa na Said Mohamed wa chuo cha Rucco aliyezawadiwa Sh.300,000, George Tito wa chuo cha Mzumbe (Morogoro) aliyeshika nafasi ya pili alipewa Sh.200,000 na Peter Patrick wa IFM aliyeshika nafasi ya tatu alipata Sh.150,000. Walter Thomson wa Mzumbe (Mbeya) alipewa Sh.100.000 kwa kushika nafasi ya nne.

Lilian Meory wa chuo cha CBE alitwaa ubingwa kwa mchezaji mmoja mmoja (wanawake) na kuzawadiwa Sh.200.000, Agnes Jacob wa chuo cha St. Augustine alishika nafasi ya pili na kuondoka na Sh.150,000, Amina Mhina wa Mzumbe (Mbeya) alishika nafasi ya tatu na kupewa Sh.100,000 na Lemi Jackson wa St.John's aliibuka katika nafasi ya nne na kupewa Sh.50.000.

Zawadi kwa washindi zilikabidhiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dionis Malinzi aliyekuwa mgeni rasmi katika fainali hizo.

Mbunge amwaga machozi Bungeni

Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita (CCM)
Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita (CCM), amedondosha machozi bungeni baada ya kukumbuka jinsi alivyolazimika kupanda kwenye mti ili kupokea simu ya msiba wa mwanae.

Mhita ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Sayansi na Teknolojia na Elimu ya Juu, katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alimwaga machozi jana wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2013/2014.

Alisema akiwa katika ziara zake katika kata ya Bereko kwenye jimbo lake 2005, aliambiwa kuwa anatafutwa nyumbani kwake.

“Wenyeji wa pale wakaniambia twende upande juu ya mti utapata mawasiliano, nikaenda na kupanda na nikaarifiwa kuwa mwanangu Najima amefariki,” alisema.

“Nakutaja mwanangu Najima huko uliko peponi kwenye kheri, mheshimiwa Naibu Spika nilipata simu ya msiba wa mwanangu nikiwa juu ya mti” alisema kwa majonzi.

Hali hiyo ilimfanya kudondosha machozi na kutoa miwani yake kabla ya kuendelea kuongea kuwa tangu mwaka 2005 hadi leo hakuna mawasiliano katika maeneo hayo, jambo linawafanya wakazi wake kupanda kwenye miti ili kupata mawasiliano.

“Namkumbuka mtoto wangu hata leo nikienda Kondoa mahali pale maana hadi leo hakuna mawasiliano,”alisema Mhita ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Huku akisisitiza haiungi mkono bajeti hiyo, Mhita,  alisema wananchi wa Kondoa Kusini wamedhalilika kwa muda mrefu na akaitaka serikali kupeleka mawasiliano katika Jimbo la Kondoa Kaskazini.

Baada ya kumaliza kuchangia wabunge wa viti maalum, Suzan Kiwanga (Chadema) na Kuruthumu Mchuchuri (CUF), walimfuata na kumfariji.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, alisema amesikitishwa na jambo hilo na kuahidi kuwa atalishughulikia tatizo hilo la mawasiliano haraka.

CHANZO: NIPASHE

JWTZ yakanusha ujumbe wa tahadhari unaosambazwa kwa simu

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema limepata ujumbe  kupitia simu za mkononi ambao umesambazwa kwa wananchi mbalimbali ukidai umetolewa na jeshi hilo.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dar es Salaam jana, ilisema ujumbe huo unasema: ‘Habari zilizotufikia hivi punde.

Mtanzania yeyote kaa makini usiokote kitu chochote ambacho una shaka nacho, kuna mabomu yamerushwa toka nchi jirani ya Malawi zaidi ya 30 zenye uzito usiopungua tani 100. Hivyo basi uonapo kitu kipo kama chupa ya chai chenye rangi ya fedha, Usiguse’.

Pia ujumbe huo unaelekeza kuwa piga namba 0756 000042 na SMS hii tuma kwa watu uwezavyo. Imetolewa na JWTZ’.

Taarifa iliyotolewa na JWTZ imewaondoa hofu wananchi kuwa ujumbe huo ni uongo na kwamba haujatolewa na jeshi hilo.

“Kwanza, Ujumbe huo haujatolewa na JWTZ.  JWTZ  haliwezi likatumia mfumo huo wa SMS kuwapa wananchi taarifa za hatari kama hizo” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa JWTZ hutangaza kupitia vyombo rasmi kama vile magazeti, radio na televisheni linapotaka kutoa taarifa kwa wananchi.

Pia taarifa hiyo ilisema kuwa bomu la tani 100 ni zito mno,  halijawahi kutengenezwa duniani na kama lipo, haifahamiki bomu hilo litarushwa vipi , kwa kutumia ndege au mzinga. 
"Lakini pia, mzinga wa aina hiyo haupo duniani kote na wala hakuna ndege yenye uwezo huo, hasa kwa bomu lenye umbile dogo kama hilo (Chupa ya Chai)," taarifa ilieleza na kuongeza:

"Tunawaomba wananchi wazipuuzie taarifa hizi kwani sio za kweli ni uongo mtupu. JWTZ lipo kwa ajili ya wananchi hivyo, kwa taarifa hizi za hatari lazima lingewajulisha kwa njia zilizoelezwa hapo juu na si kwa simu za mkononi."
CHANZO: NIPASHE

Lowassa: Tusisahau tulikotoka

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa,
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kuchangia masuala ya maendeleo katika maeneo walikotoka na sio kusubiri kurudishwa katika masanduku wakiwa marehemu.

Wito huo aliutoa jijini Dar es Salaam wakati wa harambee ya wakazi wa wilaya  ya Nyasa wanaoishi jijini Dar es Salaam, iliyolenga kukusanya Sh. bilioni moja kwa ajili ya kuchangia  maendeleo ya wilaya hiyo.

Alisema amefurahishwa na kitendo cha Wananyasa hao kujijengea utamaduni wa kushirikiana katika masuala ya  maendeleo kwa ajili ya wilaya yao.

Lowassa alisema Watanzania wengi wamekuwa hawakumbuki kufanya maendeleo vijini kwao hali ambayo inasababisha kuendelea kuwepo kwa umasikini.

“Wengi wamekuwa wakisahau kuchangia maendeleo ya sehemu walipotoka, tusisubiri mpaka turudishwe katika masanduku,” alisema.

Aidha, lowassa aliahidi kufanyakazi za maendeleo kwa kushirikiana na wannachi hao ili kufanikisha malengo yao katika eneo hilo  lililosahaulika katika sekta nyingi.

Lowasa ambaye ni Mbunge wa Monduli,  katika harambee hiyo alifanikiwa kuchangisha kiasi cha Sh. milioni 305.4, ambapo yeye binafsi pamoja na rafiki zake aliwasilisha fedha taslimu Sh. milioni 69.

Alisema aliwafuata marafiki zake na kuwaomba wamsaidie katika kufanikisha  malengo ya wilaya hiyo ambapo walimchangia Sh. milioni 49 na yeye kuamua kuongezea Sh. milioni 20.

Alisema kitendo kilichofanywa na wilaya hiyo ni jambo jema na kwamba wananchi wengine wanatakiwa kuiga mfano huo ili maendeleo yaweze kupatikana kwa haraka ikiwemo kuboresha miundombinu pamoja na huduma za afya.

Naye Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Maandalizi ya Harambee hiyo, Gilbert Zannie, alisema licha ya fursa na

rasilimali zilizopo katika wilaya hiyo iliyopo mwambao wa ziwa Nyasa, iko katika dimbwi la umasikini huku ikikosa huduma muhimu za jamii zikiwemo afya, elimu, maji  na nishati.
CHANZO: NIPASHE

Makinda ashiriki ibada ya kumwombea Mwalimu Nyerere

Spika wa Bunge, Anne Makinda
Spika wa Bunge, Anne Makinda, ameshiriki ibada ya maombi maalum kwa ajili ya kumuombea Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julisu Nyerere.

Maombi hayo yalifanyika katika mji wa Namgongo nchini Uganda yakiwa na lengo la kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa mwenye heri na hatimaye mtakatifu kulingana na na imani ya dhehebu la kikatoliki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, maombi hayo maalum hufanyika Juni Mosi kila mwaka kwa mfululizo wa siku saba.

Makamu wa Rais wa Uganda, Edward Ssekandi, ambaye alimwakilisha  Rais Yoweri Kaguta Mseven alisema mwalimu Nyerere katika maisha yake alikuwa mtetezi wa haki za wanyonge na kupigania uhuru wa Mwafrika.

Alisema Mwalimu Nyerere alijipatia sifa ndani na  nje ya nchi yake na  kwamba kamwe wananchi wa Uganda hawawezi kumsahau kwa ajili ya vita vya ukombozi wa nchi yao vya mwaka 1978 hadi 1979.

Viongozi wengine walioshiriki  ibada hiyo ni Waziri Mkuu Mstaafu, John Samwel Malecela, Mama Maria Nyerere na watoto wake watatu, akiwamo Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,  Charles Makongoro Nyerere.

Mambo motomoto Fainali tuzo za Kili


KITUO cha runinga cha ITV kitaonesha moja kwa moja fainali za tuzo ya muziki za Kilimanjaro zinazotarajiwa kufanyika Juni 8 kwenye ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema, sababu za kuichagua ITV ni kuamini wanaweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Pamoja na fainali hizo kuoneshwa moja kwa moja ITV, Kavishe alisema pia litaoneshwa sehemu tatu tofauti kwenye maeneo ya wazi. Alizitaja sehemu hizo kuwa ni Mwanza eneo la Mabatini, Temeke Uwanja wa Taifa na Kilimanjaro CCM Mkoa.
Kavishe alisema zoezi la kupigia kura wasanii kuelekea tuzo hizo zinazokwenda na kaulimbiu ya Kikwetukwetu mwaka huu lilifungwa Mei 31.
Kuhusu burudani katika usiku huo, Kavishe alisema kwamba wasanii wa sasa wataimba nyimbo za wasanii wa zamani na wasanii wa zamani wataimba nyimbo za wasanii wa sasa.

Fainali Airtel Rising Stars kuanza Julai 2

Katibu mkuu mkoa wa kisoka wa Temeke Mbarouk Mhamed (kulia) akichukua karatasi wakati wa kupanga makundi na ratiba ya michuano ya Taifa ya Airtel Rising Stars iliyopangwa kuanza Julai 2013
Fainali za Taifa za michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 za Airtel Rising Stars zimepangwa kuanza Julai 2 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam kwa mabingwa watetezi Temeke wavulana kuwakabili Kinondoni.

Akizungumza wakati wa semina elekezi ya Airtel Rising Stars 2013 iliyofanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Ofisa Maendeleo wa shirikisho hilo, Salum Madadi, alisema ARS ngazi ya mikoa imepangwa kuanza Juni 15 hadi 29.

Mikoa inayoshiriki Airtel Rising Stars mwaka huu kwa upande wa wavulana ni mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke. Mikoa mingine ni Morogoro, Mwanza na Mbeya ambapo kila mkoa unatakiwa kushirikisha timu sita. Usajili wa timu ulianza jana na utamalizika Juni 11.

Kwa upande wa timu za wasichana, alisema, mikoa itakayoshiriki ni Tanga, Kigoma na Ruvuma na mikoa yote inayoshiriki Airtel Rising Stars mwaka huu iliwakilishwa kwenye semina elekezi na makatibu wakuu ambao walipata fursa ya kupitia kanuni na taratibu za michuano hiyo ya vijana.

Upangaji wa ratiba uliofanyika leo ni wa fainali za taifa pekee kwa kuwa mashindano ya ngazi ya mkoa yataendeshwa na uongozi wa mkoa husika ikiwa ni pamoja na kupanga ratiba yake.

Kwa upande wa wasichana timu zitakazofungua dimba katika fainali za taifa ni Ilala na Kinondoni. Kwa ujumla timu 12 zitashiriki fainali za Taifa, sita za wasichana na sita za wavulana.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Meneja wa Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mbando alitoa rai kwa makatibu wakuu wa mikoa kuwa makini wakati wa usajili ili kupata vijana wenye vipaji ambao wataiwakilisha vema Tanzania kwenye michuanoa ya kimataifa ya Airtel Rising Stars.

Vile vile Tanzania itawakilishwa kwenye kliniki itakayofanyika chini ya makocha wa Manchester United.

Alisisitiza alisema nia thabiti ya Airtel Tanzania kuendelea kusaidia mashindano ya vijana kwa nia ya kuendeleza soka nchini na kuishukuru TFF na wizara inayohusika na michezo kwa kuyaunga mkono mashindano hayo.

Naye mgeni rasmi katika semina  hiyo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Msafiri Kondo aliwaomba wadhamini kuendelea kudhamini michuano hiyo ili vijana wa kike na kiume waweze kufikia malengo yao katika soka.

Blog Archive

Popular Posts

.

CHAT BOX

My Blog List

 
Support : BONGOCLANTZ
Copyright © 2013. KANGAROO - All Rights Reserved
Template Created by EDDIE SUCRE
Proudly powered by Blogger