Home » » Kombe la Kagame Sudan majanga

Kombe la Kagame Sudan majanga

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unatarajia kukutana kujadili hatua za kuchukua baada ya serikali kuzionya timu za Tanzania kwenda Sudan kushiriki michuano ya soka Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kutokana na hofu ya usalama.

Akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bungeni, Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe alisema kuwa hali ya usalama mjini Darfur ambako michuano hiyo imepangwa kufanyika ni ya wasiwasi kwa sababu watu wanaokwenda huko wanapokewa na vikosi vya magari yasiyoingia risasi na huvishwa nguo ambazo hazipenyezi risasi.

Akizungumza katika kipindi cha Spoti cha Radio One jana usiku, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kuwa wamepanga kukaa kujadili tamko hilo la serikali.

Osiah alisema kuwa uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ukiongozwa na rais wa shirikisho hilo, Nicholaus Musonye waliwahakikishia usalama nchini Sudan na kwamba kabla ya kuamua michuano hiyo ifanyike nchini humo, walienda kukagua miundombinu itakayotumika.

“Shirikisho lolote la soka huwasiliana na serikali ya nchi husika kujua hali ya usalama kabla ya kuandaa mashindano. Viongozi wa CECAFA walienda kukagua viwanja Sudan wakaridhia michuano ya Kagame ifanyike huko,” alisema Osiah.

“Kwa kuwa serikali yertu (Tanzania) imeingiwa na hofu kuhusu usalama wa Sudan, itabidi sisi (TFF) tukae tuamue hatua ya kuchukua,” aliongeza.

Michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu imepangwa kuanza Juni 18 na kumalizika Julai 2 nchini humo. Mabingwa watetezi Yanga, Simba na Super Falcon ya Zanzibar zinataraji kushiriki katika michuano hiyo ambayo imepangwa kucheza katika vituo viwili vya Alfashery kilichopo Darfur kaskazini, na Kadugli.

Wakati huo huo, uongozi wa Simba umesema hauko tayari kushiriki michuano hiyo endapo CECAFA haitabadili vituo vya kufanyika kwake.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa na kituo cha redio cha jijini Dar es Salaam akidai kuwa hali ya usalama nchini Sudan si shwari.

0 comments:

Post a Comment

Blog Archive

Popular Posts

.

CHAT BOX

My Blog List

 
Support : BONGOCLANTZ
Copyright © 2013. KANGAROO - All Rights Reserved
Template Created by EDDIE SUCRE
Proudly powered by Blogger