Idadi
ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana
imeongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la
Taifa (Necta), kufanya marekebisho alama za viwango vya ufaulu,
Mwananchi limebaini.
Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema matokeo hayo ambayo
yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na kufikia asilimia kati ya 54 na
57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale ya kidato cha sita
ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari kutoka Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha
kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka
asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa awali na huenda yakafikia
asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao 82,000 ambao
awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa wamepanda na
kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.
Kwa matokeo hayo, watahiniwa wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri
kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 ya
349,390 waliofanya mtihani huo walifaulu.
Msemaji wa Necta, John Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa
bado unaendelea. “Ninachojua kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na
matokeo yatatangazwa mapema tu ili watoto waweze kujiunga na shule
mapema,” alisema Nchimbi.
Pia alisema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya awali
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dk Shukuru Kawambwa yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756
waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa
daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 126,847 sawa na asilimia 6.4.
Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa na asilimia 28.1.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata
sifuri, hesabu ambayo imebadilika katika matokeo mapya ambayo
yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja hilo ni 158,100 ambayo ni
asilimia 43.
Hata hivyo, habari kutoka Necta zinasema kuwa licha ya kuwezesha
kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya kanuni mpya ya kukokotoa matokeo
hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500 kushuka ufaulu
ikilinganishwa na awali.
Maofisa mbalimbali wa Necta pamoja na wale wa Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi na taasisi zake, walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita
kukubaliana masuala mbalimbali juu ya matokeo hayo pamoja na suala la
matokeo ya wanafunzi hao 2,500 kabla ya kutangazwa wiki hii.
“Baada ya wajumbe kujadili suala lile, busara ilibidi itumike kwa hiyo
hakuna mwanafunzi ambaye alama yake itashuka, kwa kawaida isingewezekana
mtoto ambaye matokeo yalitoka akiwa amefaulu leo umwambie ameshuka,”
kilieleza chanzo chetu.
Matokeo
ya awali ndiyo chimbuko la kupitiwa upya baada ya wadau kuyalalamikia
na kumlazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume ya kuyachunguza
Februari 23, mwaka huu.
Kabla
ya tume hiyo kuhitimisha shughuli zake, ilitoa taarifa ya awali ambayo
ilipendekeza kufutwa kwa matokeo hayo kwa maelezo kwamba Necta ilitumia
kanuni mpya ya kukokotoa matokeo bila kushauriana na wadau.
Serikali
ilitoa taarifa bungeni kwamba imeamua kufuta matokeo ya 2012 na kuamuru
yapangwe upya kwa kufuata madaraja yaliyotumika mwaka 2011.
Home »
magazeti
» HII NI NEEMA KWA WALIOFELI KIDATO CHA NNE....UFAULU WAONGEZEKA, MATOKEO NI MUDA WOWOTE
HII NI NEEMA KWA WALIOFELI KIDATO CHA NNE....UFAULU WAONGEZEKA, MATOKEO NI MUDA WOWOTE
Posted by Unknown
Posted on 12:30 PM
with No comments
0 comments:
Post a Comment